Wadau katika masuala ya uimarishaji wa vijana wameshinikiza Kenya na Afrika kuwekeza zaidi katika vijana kwa kuwapa nafasi za uongozi na ujuzi mbalimbali ili kutambua uwezo wao katika jamii.
Wakizungumza mjini Mombasa katika Kongamano la The Duke of Edinburgh’s International Award Foundation kwa ushirikiano na The President Award-Kenya, wadau hao wamesema Afrika inakadiria kuwa na idadi ya vijana milioni 830 ifikapo mwaka wa 2050, hivyo basi kuimarishwa kwao kutafanikisha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo katika Bara Afrika.
Katika kongamano hili vijana wakiongozwa na Solidad Mwangeni kutoka Shule ya Upili ya Wasichana St. Thomas Kilifi walipata nafasi kuonyesha vipaji vyao vilivyochochewa kupitia ushirikiano wa The Duke of Edinburgh’s International Award Foundation na kitengo kilichoko chini ya Wizara ya Michezo na Tamaduni nchini -The Presidents Awards Kenya.
Mwenyekiti wa The Duke of Edinburgh’s International Award Foundation ambaye pia ni mmoja wa wasimamizi (trustee) wa wakfu huo Muhoho Kenyatta amesema kunawiri kwa Bara Afrika na taifa la Kenya kwa ujumla kunategemea vipi mataifa yataimarisha vijana wake.
Waziri wa Michezo Salim Mvurya amesema kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali -wanalenga kubuni sheria na mikakati itakayoimarisha mazingira bora ya vijana kujiendeleza, mikakati ambayo imeungwa mkono na katibu katika wizaya yake Fikirini Jacobs.
Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir amewataja vijana kama nguzo muhimu katika uimarishaji wa uchumi, huku Katibu Mkuu katika wakfu wa The Duke of Edinburgh’s International Award Foundation Martin Houghton Brown akisema wakfu huo unalenga kunufaisha vijana milioni 1.3 Afrika katika kipindi cha miaka mitatu.